Bible Study: FrontPage




 

1 Samweli, Chapter 23

Bible Study - 1 Samweli 23 - Swahili - Swahili Union Bible - Web
 
 
 
Comment!       Comment Disqus!
  
1. Kisha wakamwambia Daudi, kusema, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka sakafuni mwa kupuria.
  
2. Basi Daudi akamwuliza Bwana, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye Bwana akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila.
  
3. Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti?
  
4. Basi Daudi akamwuliza Bwana tena, Naye Bwana akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako.
  
5. Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng'ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila.
  
6. Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake.
  
7. Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo.
  
8. Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumhusuru Daudi na watu wake.
  
9. Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera.
  
10. Ndipo Daudi akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu.
  
11. Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye Bwana akamjibu, Atashuka.
  
12. Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? Bwana akasema, Watakutia.
  
13. Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda po pote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje.
  
14. Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake.
  
15. Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi.
  
16. Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu.
  
17. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu.
  
18. Na hao wawili wakafanya agano mbele za Bwana; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake.
  
19. Ndipo wale Wazifi wakakwea kwa Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha kwetu ngomeni mwa Horeshi, kilimani pa Hakila upande wa kusini wa Yeshimoni?
  
20. Basi sasa, Ee mfalme, ushuke, kama utakavyo nafsini mwako kushuka; na kazi yetu itakuwa kumtia mkononi mwa mfalme.
  
21. Naye Sauli akasema, Na mbarikiwe ninyi na Bwana; kwa sababu mmenihurumia.
  
22. Nendeni, nawasihi, mkazidi kupata hakika, mkajue na kuona mahali pake anapojificha, tena ni nani aliyemwona huko; maana nimeambiwa ya kwamba atenda kwa hila nyingi.
  
23. Chunguzeni basi, mkayajue maficho yake yote anapojificha; kisha njoni kwangu, tena msikose, nami nitakwenda pamoja nanyi; tena itakuwa, akiwapo katika nchi, mimi nitamtafuta-tafuta katika elfu zote za Yuda.
  
24. Nao wakaondoka, wakaenda Zifu kumtangulia Sauli; lakini Daudi na watu wake walikuwapo nyikani pa Maoni, katika Araba upande wa kusini wa jangwa.
  
25. Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni.
  
26. Sauli akaenda upande huu wa mlima, na Daudi na watu wake wakaenda upande huu wa mlima; naye Daudi akafanya haraka sana kwenda zake kwa hofu ya Sauli; kwa sababu Sauli na watu wake wakamzunguka Daudi na watu wake ili kuwakamata.
  
27. Lakini akaja mjumbe kwa Sauli, kusema, Njoo upesi, kwa kuwa Wafilisti wameishambulia nchi.
  
28. Basi Sauli akarudi kutoka kumwinda Daudi, akaenda kinyume cha Wafilisti; kwa hiyo wakapaita mahali pale, Selahamalekothi.
  
29. Naye Daudi akakwea kutoka huko, akakaa katika ngome ya Engedi.


Search in:
Terms:

Vote and Comment on Facebook:Recommend This Page:
Post on Facebook Add to your del.icio.us Digg this story StumbleUpon Twitter Google Plus Post on Tumblr Add to Reddit Pin this story Linkedin Google Bookmark Blogger
Insert Your Personal Insight:

Please do not make mean comments and follow the biblical and spiritual character of this forum. If, however unpleasant situations arise, we request to flag it to us in order to evaluate the situation.

Text source: This text is in the public domain, downloaded from http://www.unboundbible.org, compiled by biblephone2008@gmail.com.

This project is based on delivering free-of-charge the Word of the Lord in all the world by using electronic means. If you want to contact us, you can do this by writing to the following e-mail: bible-study.xyz@hotmail.com


SELECT VERSION

COMPARE WITH OTHER BIBLES