Bible Study: FrontPage




 

Matendo ya Mitume, Chapter 17

Bible Study - Matendo ya Mitume 17 - Swahili - Swahili Union Bible - Web
 
 
 
Comment!       Comment Disqus!
  
1. Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi.
  
2. Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu,
  
3. akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo.
  
4. Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache.
  
5. Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji;
  
6. na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,
  
7. na Yasoni amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu.
  
8. Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo.
  
9. Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao.
  
10. Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.
  
11. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.
  
12. Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache.
  
13. Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawachafua na kuwafadhaisha makutano.
  
14. Mara hiyo wale ndugu wakampeleka Paulo aende zake mpaka pwani; bali Sila na Timotheo wakasalia huko.
  
15. Lakini wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao.
  
16. Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake.
  
17. Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku.
  
18. Na baadhi ya Waepikureo na Wastoiko, wenye ujuzi, wakakutana naye. Wengine wakasema, Mpuzi huyu anataka kusema nini? Wengine walisema, Anaonekana kuwa mtangaza habari za miungu migeni, kwa maana alikuwa akihubiri habari za Yesu na ufufuo.
  
19. Wakamshika, wakamchukua Areopago, wakisema, Je! Twaweza kujua maana ya elimu hii mpya unayoinena?
  
20. Kwa maana unaleta mambo mageni masikioni mwetu, tutapenda kujua, basi, maana ya mambo haya.
  
21. Kwa maana Waathene na wageni waliokaa huko walikuwa hawana nafasi kwa neno lo lote ila kutoa habari na kusikiliza habari za jambo jipya.
  
22. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.
  
23. Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.
  
24. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono;
  
25. wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.
  
26. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;
  
27. ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.
  
28. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.
  
29. Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu.
  
30. Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu.
  
31. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.
  
32. Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo.
  
33. Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha.
  
34. Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao.


Search in:
Terms:

Vote and Comment on Facebook:Recommend This Page:
Post on Facebook Add to your del.icio.us Digg this story StumbleUpon Twitter Google Plus Post on Tumblr Add to Reddit Pin this story Linkedin Google Bookmark Blogger
Insert Your Personal Insight:

Please do not make mean comments and follow the biblical and spiritual character of this forum. If, however unpleasant situations arise, we request to flag it to us in order to evaluate the situation.

Text source: This text is in the public domain, downloaded from http://www.unboundbible.org, compiled by biblephone2008@gmail.com.

This project is based on delivering free-of-charge the Word of the Lord in all the world by using electronic means. If you want to contact us, you can do this by writing to the following e-mail: bible-study.xyz@hotmail.com


SELECT VERSION

COMPARE WITH OTHER BIBLES